NILIPOTEA! PART 5 - SEHEMU YA ‘A’.
Wasiwasi ulianza kumpata mama Penny baada ya week ya pili kuanza bila kumsikia Tunda. Mumewe alimtuliza na kumwambia walihitaji huo muda. Wawaache tu. “Tunda sio mtu wa kukaa zaidi ya week bila kunitafuta! Mimi namjua yule. Maswali yake huwa hayaishi.” “Basi ujue safari hii kapata wakumuuliza.” Mama Penny akacheka. “Na kweli.” Wakataniana hili na lile. Wakaacha.
Mama yake na wadogo zake walishahamia
kwenye nyumba ndogo aliyokuwa amelipiwa na Tunda. Na kwa kuwa nyumba ya Net
ilikuwa imejaa, Tunda akaamua kumpa mama yake vitu vyake vyote vya ndani,
kasoro nguo zake na vitu vyake vingine, alivihamishia kwa mama Penny. Hata gari
yake aliiacha nyumbani kwa mama Penny. Kuwa wakitoka kwenye fungate ndipo aende
akachukue vitu vyake vyote ahamie nyumbani kwa Net, ambapo ndio ilikuwa nyumba
yake. Alishaachia nyumba aliyokuwa akiishi.
Vita ya wenyewe
kwa wenyewe. Kwa Bethy na Gabriel.
Ni miluzi ya Gabriel tu ndio iliyokuwa
ikisikika ndani ya nyumba yake mchana na usiku. Furaha ilimjaa, usingemsikia
akibishana na Bethy tena mpaka Bethy akawa anashangaa. Akianzisha kelele,
Gabriel anaongeza sauti ya tv, au anatoka nje kabisa. Bethy akimjia kwa heri,
basi Gab atamjibu kwa ufupi na kuondoka kabisa pale kama anayemkwepa.
Usingemkuta nyumbani kama watoto wake hawapo. Bethy akawa haelewi mwisho wa ile
hali ni nini asijue linalomkabili.
Baada ya majuma mawili tokea Net aondoke,
na ukimya ukiwa ndani ya nyumba yao, Bethy akiwa ofisini kwake, akaambiwa ana
mgeni. Akiwa hamfahamu mgeni mwenyewe, akamwambia sekretari wake amruhusu
aingie ndani. Yule mtu alijitambulisha kama ni mwanasheria aliyetumwa na
Gabriel, anatakiwa asaini makaratasi ya talaka.
Nusura Bethy aanguke. Alichofanya
nikuchukua zile karatasi zote, pochi na funguo zake za gari akatoka ofisini
kwake na kumuacha yule mwanasheria amekaa pale pale, yeye akaenda mpaka ofisini
kwa mumewe.
Alimkuta Gabriel na wageni watatu
ofisini kwake, akaingia bila hata hodi. Akamtupia Gabriel zile karatasi usoni
mbele ya wageni wake. “Naona umepata ujumbe wako.” Gabriel alimkejeli huku
akijaribu kukwepa zile karatasi, na cheko la kejeli juu kwa mkewe. “Kama
unafikiria kuniacha mimi ili umuoe malaya wako, ujue yupo jela. Anakabiliwa na
makosa ambayo hawezi kupewa dhamana.” Palepale uso wa Gabriel ukabadilika.
Akasimama.
“Unasemaje
Bethy!?” Bethy akaanza kumcheka. “Wewe huoni mjini kulivyo na amani? Kila
mwenye ndoa yake ametulia kwake na familia yake! Sababu malaya wa jiji yupo
selo. Na hatoki kwa dhamana wala hongo. Ndio ujue waliokutangulia mjini
wamekutangulia. Sasa vimba, upasuke. Hata ukiniacha mimi, ujue na wewe
umekosa.” Bethy akatoka huku anamcheka mumewe. Hasira na mshtuko vilimfanya
aropoke kitu alichokuwa ameonywa sana na Ritha.
Gabriel kwa
Ritha.
Hapo hapo akawaaga wale wageni nakutaka
watoke ofisini mwake. Akampigia simu mama Cote. “Ni nini
kinaendelea kwa Tunda?” “Sijui. Kwani vipi!?” Ritha akajibu kwa
kujiamini. “Nisikilize mama Cote. Usithubutu kunichezea akili.
Hakika nakuonya. Kama unanichezea au ulinigeuka, hakika utajuta. Nilihakikisha
unanielewa kabla hatujaanza mchakato…” “Tulia kwanza Gabriel. Kwani kuna nini?”
Ritha akajifanya hafahamu chochote. “Bethy ameniambia kila kitu.”
Gabriel akaamua kumtega.
“Sio mimi ninayehusika Gabriel.
Ni mkeo. Kama amenisingizia mimi, basi ujue nimuongo. Yeye ndiye aliyetaka
kumshitaki Tunda. Ndiye aliyewasiliana na mfanyakazi wa kampuni ya simu na
kumuomba amtolee mawasiliano ya Tunda ya miaka mitatu mpaka minne iliyopita.
Jumbe na malipo yote aliyokuwa akipokea kwa biashara ya ngono aliyokuwa
anafanya. Ame..” “Nakupa nafasi ya mwisho mama Cote. Una uhakika kabisa
hauusiki na kumuweka Tunda ndani? Sitakusamehe na utalipa kwa kunizunguka. Na
nitahakikisha unalipa kwa machungu. Sikudanganyi.” Gabriel
alikuwa akitetemeka kwa hasira, hakutaka maneno mengi, akamkatisha Ritha
kumtaka ukweli. Kimya. “Mama Cote?” Gabriel akaita, mara akasikia simu
imekatwa.
Gabriel alitoka pale kama
aliyechanganyikiwa akaenda mpaka kituo cha polisi Kawe. Hakumkuta mkuu wa kituo
ambaye ni rafiki yake. Akajaribu kuulizia pale ili kujua alipowekwa Tunda.
Hakupata majibu yakumridhisha. Akaamua kumpigia simu mkuu wa kituo, akamwambia
atakuwepo hapo ofisini baada ya kama masaa mawili. Huo muda ulikuwa mrefu sana
kwa Gabriel, akatoka tena pale mpaka ofisini kwa mama Cote. Hakumkuta.
Sekretary wake akamwambia kuwa alitoka, bila kumuaga. Alipojaribu kumpigia,
simu zake zote tatu zilikuwa zimefungwa.
Gabriel kwa Bethy
Gabriel akatoka pale ofisini kwa Ritha
mpaka ofisini kwa mkewe. “Nimeambiwa wewe ndio umemshitaki Tunda.” “Nisikilize
Gab. Kama mmezungukana na mama Cote, mimi hayanihusu. Sijui makubaliano yake na
wewe, ila najua yangu na yeye. Tulipeana majukumu kama alivyofanya na wewe. Kwa
kuwa mimi nafahamiana na mtu wa kampuni ya simu, nimepata ushahidi nilioutaka,
na yeye ametafuta shahidi wa kukiri
kufanyiwa biashara ya ngono na Tunda. Sasa sijui.” “Nani?” Gab akauliza.
“Wewe
unawazimu nini Gabriel!? Ni kwambie ili iweje!?” Bethy akamshangaa sana. “Wewe
shida yako ilikuwa mfanikishe na mama Cote, Net atoke nchini na asirudi tena.
Mmetengeneza kesi yenu, mmefanikiwa. Mimi shida yangu ilikuwa kumuweka Tunda
mbali na familia yangu. Anakuwa wapi, mimi sikujali ilimradi iwe mbali.” Gabriel alitulia kabisa
akimsikiliza mkewe. Alimjua jinsi alivyo mropokaji anapokuwa na hasira. Kwa
hiyo akajua atayasema yote.
Bethy naye akaendelea bila shida
akitaka kumuumiza zaidi. “Sasa kwa kuwa na shida ya mama Cote ilikuwa pia
kumkomoa Tunda, na arudishe mali zake, basi, tukaunganisha nguvu, na sisi
tukapanga mipango yetu, tumefanikiwa. Ushahidi wa kumshitaki Tunda, upo. Tena
sio magumashi. Upo ushahidi kabisa na wa uhakika. Tunasubiri siku ya kesi yake
mwanasheria awakilishe ushahidi, ahukumiwe makosa yake, afungwe jela atupishe
wenye ndoa zetu mjini.” Na kweli Bethy aliongea yote.
Gabriel akatoa simu yake akaanza
kumpigia tena simu mama Cote zaidi ya mara mbili hakumpata. Bethy akazidi
kumcheka. “Tena kwa taarifa yako tu, huyo malaya wako atahukumiwa kwa haraka
sana ili msije kumtoa. Hiyo pesa iliyomwagwa ili kuendesha kesi yake kwa
haraka, hakika hatoki. Anza kutulizana kwenye ndoa yako.” “Nishamalizana na
wewe Bethy. Wazazi wangu wanajua wewe si mke wangu. Nasubiri kukamilisha tu
taratibu kisheria, maisha yangu yaendelee.” Bethy akashtuka sana. Kwamba mpaka
wazazi wake Gab wanajua!
Bado Gabriel alikuwa amesimama. Macho
kwenye simu.“Namuhurumia mama Cote!” Gabriel aliongea huku akijaribu kumpigia
tena. “Hakika atajuta kwa kunigeuka!” “Hebu subiri kwanza wewe Gab. Yaani
hasira hiyo ni kwaajili ya kuwekwa ndani malaya
yule!” Gabriel akatoa macho kwenye simu na kumtizama mke wake, akacheka kwa
kuguna.
“Haupo hata
robo ya Tunda.” “Kwa kipi!? Nimesoma kuliko yeye. Nina..” “Kama ndoa inajengwa
na shule, mbona wewe mwenye madigirii mengi imekushinda!? Mume mmoja tu na
watoto wawili wanakushinda kuwatuliza na kuwafanya walale hata usiku mmoja tu
kwa amani! Umejawa kelele! Fujo tupu. Usijifananishe na Tunda hata kidogo.
Nakujua wewe na Tunda, ndani na nje. Yeye unamwita malaya, lakini
nakuhakikishia Bethy, haupo hata robo yake. Wala usithubutu kujilinganisha
naye. Nikujidhalilisha. Kajaribu kwa wasio kufahamu.” Gabriel aliongea taratibu
tu bila jazba. Bethy akazidi kucharuka.
“Na usiku wa
leo, usirudi nyumbani. Nitamwambia dereva akupelekee mizigo yako kwenye kile
kijinyumba chako ulichokuwa ukininyanyasa nacho. Angalau usiku wa leo uishe kwa
amani kwangu. Umekuwa adhabu!” “Ujue ukinifukuza mimi naondoka na watoto.”
Bethy akamtisha.
“Ukitaka
nenda kawafuate shule hata sasa hivi. Ila ujue kabisa, ukiwatoa kwangu,
unawatunza.” Gabriel alijibu bila hata wasiwasi, akarudisha macho kwenye simu.
“Kweli Gab!?
Na hayo yote ni sababu ya Tunda, malaya yule!” “Malaya aliyeniheshimu na kunihudumia
wakati wewe umeshindwa. Na pili, sitakusamehe kwa kunigeuka. Nisikuone nyumbani
Bethy. Kama umeamua kuchukua watoto, niambie sasa hivi na wao wafungashiwe
mizigo yao.” Bethy hakuamini.
“Wewe
umelogwa Gabriel. Unatelekeza watoto sababu ya upumbavu huo?” “Sitatelekeza
wanangu! Wewe vipi Bethy!? Si watakuwa na wewe, mama yao! Una kazi nzuri na
uwezo wakuwalea unao. Pili, umenigeuka, sio upumbavu. Kama umeweza kufanya
mpango mkubwa hivyo mpaka ukafanikiwa kumuweka Tunda ndani, unafikiri
anayefuata ni nani kama sio mimi?” “Siwezi kukufanyia hivyo Gab, wewe ni mume
wangu. Nimefanya yote kwa ajili yako. Nataka tubaki kwenye ndoa yetu.” Gafla
Bethy akajirudi.
“Hivi unajua
unazungumza na mimi sio mtu mwingine?” “Najua.” “Sasa mbona unaongea mambo
ambayo hata wewe mwenyewe yanakuwia vigumu kutoka mdomoni mwako! Acha ujinga
Bethy. Na ujipange. Umeanzisha jambo ambalo, litakurudi tu. Mwenzio amekimbia
hata kwenye simu hapatikaniki. Na kama unafikiri umemkomoa Tunda, ujue nitamtoa
tu na wewe utaweka saini kwenye talaka. Nakushitaki kwenye vyombo vya sheria.
Na hivi ninavyokwambia nakwenda kutafuta njia yakumtoa Tunda. Hana kosa la
jinai linaloshindikana kuwekewa dhamana.” Gabriel akaangalia muda, akatoka.
Bethy akamkimbilia nje. “Huwezi kumtoa
Tunda.” Akamshika shati kwa nguvu. “Sijakugusa Bethy, na wewe usiniguse. Acha
kunidhalilisha mbele za watu.” “Unaona haya kwa lipi wakati wewe umeamua kuacha
familia yako ili ukaishi na malaya anayejiuza hapa mjini!? Mama Cote
amekusaidia kukutengenezea kesi nzuri tu ili kumdhibiti na akili yako itulie
kwa familia yako na wewe unaenda kumtoa!”
Bethy akaanza kuongea kama amerukwa na akili.
“Wala Tunda
hakuwahi kukupenda Gab. Hata yeye alikuja kukutamkia wazi hakukuficha.
Alikuomba umuache, sasa hivi ameamua kutulia na maisha yake. Alikwambia wewe ni
muhanga kama wahanga wengine aliowatumia kujinufaisha na maisha aliyoishi
zamani. Alikuwa akikutumia tu. Kwa nini unashindwa kuelewa hilo wakati alikiri
kwako wazi na kukutaka umuache na usimtafute tena?”
“Kama mnajua
hilo ni kwa nini mmemtengenezea kesi ili afungwe!? Nilimuacha Tunda wakati ule
akiwa na shida, tena ananililia shida. Akiwa na njaa, nilimtupa, ili nitulie
nyumbani na wewe Bethy. Ulibadilika?” “Wewe ndio hukubadilika Gab. Ulimuacha
Tunda kwa matendo, lakini akili zako hazikuwa nyumbani.” “Ulitaka nifanye nini
kwako ambacho nilishindwa kufanya na wewe ukashindwa kubadilika!?” Gabriel
akamuuliza mkewe taratibu tu.
“Akili zako
zilikuwa kwa Tunda.” “Ndio shida yako Bethy, na wewe ni muongo. Tangia
tukubaliane nimuache Tunda, mbele ya mchungaji, sema ukweli, nilishamtaja hata
mara moja kwako?” Kimya. “Wewe ndio unajishuku na kunifuatilia hata kwenye
mambo ya msingi! Kila mahali wewe ni wivu na ugomvi. Kila ujumbe unataka kusoma
wewe! Unataka kutawala ambako huelewi wala huwezi! Unataka kuwa bosi wa
wafanyakazi ambao hufanyi nao kazi! Wewe umeajiriwa na umesoma, umeona wapi huo
utaratibu? Huwezi kuwa bosi wa biashara zangu!” Gabriel akaendelea. Taratibu
tu.
“Huwezi
kunizuia na kutaka ujue na kuelewa kila mtu ninaye zungumza naye wakati wewe
unajua mimi ni mfanyabiashara! Nafanya biashara na wanawake na wanaume. Mimi
sichagui. Popote pesa ya halali ilipo, naifuata. Lakini wewe unashindwa
kuniamini, na hutaki kuelewa. Nikiishiwa unashindwa hata kunipa nauli ya
daladala au hutaki nitumie hata gari yako! Sasa ulitaka nifanye nini? Nikae
nyumbani uendelee kuninyanyasa kuwa sina akili?” Gabriel aliendelea kumuhoji
bila jazba.
“Mbona
ulitembea na Tunda? Tena sio kutembea naye mara moja! Ni kuwa na mahusiano
naye!?” “Nilikujibu wewe na mchungaji. Ni wewe mwenyewe ulinifikisha kwa Tunda,
na nilikuonya usimlaumu Tunda. Nilihitaji msaada ambao ulishindwa wewe kunipa,
akanipa Tunda. Ulitaka nikubembeleze mpaka lini? Hukuwahi kunithamini
nilipokuwa na shida, mpaka sasa nimefanikiwa pia bado hunithamini.”
“Narudia
tena. Haupo hata nusu ya Tunda. Na Tunda siye aliyenifanya nikuache wewe, wala
hakunitongoza. Mimi mwenyewe nilimtaka Tunda. Sikuwahi kuwa na mahusiano yeyote
na yeyote isipokuwa wewe. Niliapa kuwa mwaminifu kwako, lakini wewe ukanitesa
ukijua sina pakwenda. Nilimpata Tunda, nikamuomba awe na mimi. Akakubali na
kuniheshimu sana. Narudia tena, sijui ilikuwaje kwa wengine, lakini mimi najua
kwa upande wangu, ndiye niliyemuhitaji Tunda, na nikatulia kwa kuwa aliweza
kunipa kile ulichoshindwa wewe kunipa.” “Alikukubali sababu ya pesa tu. Hakuna
lolote, wala si mapenzi.” Bethy akajibu kama kumshushua.
“Kwani mimi
nakataa! Nilimuacha, na nilihakikisha ananufaika na pesa yangu, kwa kuwa na
mimi nilikuwa nanufaika zaidi na yeye. Tunda alinifanya nitulie nakuweza
kufikiria zaidi na nikaweza kutengeneza pesa zaidi. Heshima, utulivu na uwezo
wa kunisikiliza kutoka kwa Tunda vilinifanya nitulie hata wakati wewe ulipokuwa
ukininyima usingizi tukiwa wote, Tunda alinituliza nyumbani.”
“Na kwa
taarifa yako tu, Tunda hakuwahi hata mara moja kunishauri nikuache. Wakati wote
alikuwa akinituliza ili mimi na wewe tuweze kulea watoto. Tunda anajua umuhimu
wa ndoa. Hakutaka watoto wangu wakue bila wewe au mimi. Wakati wote alinitaka
nijaribu kutafuta jinsi yakuweza kuishi na wewe kwa amani na utulivu.
Akinishauri hili na lile, pengine kutakuwa na amani.” “Alikushauri nini kama
sio uongo?” Bethy akauliza kwa jazba.
“Ni mengi
Bethy. Mengi mno. Tena alikuwa akinifuatilia kama nimekufanyia ili kuleta
amani, lakini pia ilishindikana. Tunda hakuwa malaya kwangu. Alikuwa rafiki
ambaye sikuwa na sababu yakujificha kwake. Niliongea mbele yake kwa uwazi
kabisa na yeye alinishauri akitaka nitulie kwako. Lakini ilishindikana Bethy.
Ulinitoa kwa Tunda, tena ukakataa hata nisiwasiliane naye kwa salamu tu!
Nikakubali. Nikatulia nyumbani, lakini wewe hukuwahi kubadilika Bethy. Ukawa ni
kama umenitoa kwenye heri, nakunitupa kwenye dhiki, ambako ni kwenye nyumba
niliyojenga mwenyewe.”
“Ulishindwa
ndoa wewe mwenyewe. Huna wakumlaumu. Wewe mwenyewe na roho yako mbaya, ndio
ulimrudisha Tunda kwangu. Wewe mwenyewe ili tu kumuumiza Tunda. Hakunitafuta
wala sikumtafuta. Ukanipa namba zake za simu, na kutaka nipange naye miahadi
tukutane ili kuhakikisha kama Tunda amebadilika kweli. Unakumbuka fujo
ulizofanya kunilazimisha nimtafute tena Tunda mpaka nikakubali kumtafuta tena
Tunda, tena ukiwa umenisimamia kuhakikisha namtafuta Tunda ili mumchafue
kuhakikisha hajabadilika? Unakumbuka Bethy au umesahau?” “Nilitumwa na mama
Cote.” Akajaribu kujitetea.
“Kwa fujo
zile zakuamsha nyumba nzima, mpaka watoto na kunifuata mpaka kazini kwa kelele
nyingi ili nimtafute Tunda!? Ni mama Cote peke yake au alikuwa akikusaidia
kukujaza ujinga tu. Ulimrudisha Tunda kwangu, wewe mwenyewe ukisaidiwa na mama
Cote bila kufikiria sababu ya hila zenu kwa mtu ambaye hata hakuwa na habari na
nyinyi.”
“Na Mungu
naye akawapa mlango wa kwanza wakutokea, ili mumuache Tunda. Mkanivalisha
spika. Mkasikia mazungumzo yetu yote na Tunda. Akajibu Tunda bila hila. Tena na
wewe ukisikia jinsi alivyokuwa akinishauri nitulie nyumbani, nikurudie wewe
bila kujua mateso niliyokuwa nikipitia tokea ututengenishe naye. Umesahau hata
hilo!? Eti Bethy?” “Ule ulikuwa ni unafiki tu. Hana lolote. Kama yeye anajua
sana ndoa, mbona asiolewe sasa, tukamuona ametulia kwenye ndoa yake?” Gabriel
akatingisha kichwa kama anayemsikitikia mkewe.
“Sasa
nakuonya Bethy, kwa kuwa Mungu mwenyewe aliwapa mlango wakutokea,
hamkumsikiliza Mungu mkaendelea kumkaidi kwa kumfuatilia Tunda ambaye
alishajitenga na nyinyi na akakiri amebadilika, lakini bado mkaendelea
kumfuatilia. Sasa mwambie na mama Cote, mchezo mliomfanyia Tunda, sitauruhusu.”
“Tunda yupo jela kwa makosa sahihi. Tulichokifanya sisi ni kutafuta ushahidi tu
na kumpeleka kwenye vyombo vya usalama.” Bethy akajibu kwa jeuri.
“Na ushahidi
upo wa uhakika. Mwanamke wako hatakaa atoke jela.” “Basi tutashindana
mahakamani. Kusanyeni ushahidi wenu wote. Wewe na mama Cote, mwanamke aliyejawa
uchu wa mali, yupo tayari hata kumuangamiza mtoto wake sababu ya mali!” “Sio
mali, hataki mtoto wake aoe changudoa.” Bethy akatetea.
“Tunda
ameokoka, ametubu dhambi zake, amesamehewa. Nyinyi ndio mmemtoa kanisani, na
kumpeleka jela. Na Mungu hatawaacha.” “Kama yupo kanisani mbona unamfuata?”
“Kwani wewe nilikutoa wapi? Si kanisani? Ndivyo nitakavyofanya kwa Tunda.
Utasaini makaratasi ya talaka, namuoa Tunda kama nilivyokuoa wewe, na mimi
nipumzike na kutulia na Mungu wangu. Wewe ni shetani utakayeniingiza kuzimu. Na
leo ni mara ya mwisho kubishana na wewe Bethy. Tutahamia kwenye vyombo vya
sheria, watuhukumu kwa haki. Nimechoka na wewe mwanamke mbaya kuliko shetani!
Mwishowe utanifanya kama mlichomfanya Tunda.” Gabriel akaendelea.
“Na mwambie
mama Cote, tukimalizana na kesi ya Tunda, naanza kumfungulia na yeye mashitaka.
Mwambie nafahamu mabaya yake yote. Sasa naenda kumtoa Tunda jela, ili tumpe
mama Cote nafasi. Maana kwa serikali hii, lazima wamfunge tu.” Gabriel alipoona
watu wanazidi kukusanyika pale waliposimama huku wakiwachukua video, na mmoja
wa askari anayelinda lile jengo anawasogelea, akaamua aondoke. Ili wasije
kutoka kwenye mitandao.
“Na kwa
taarifa yako Tunda hawezi kutoka kwa dhamana.” Gabriel akamgeukia mkewe. “Kwani
Tunda ameua? Amefanya Money laundary? Ameuza madawa ya kulevya? Anakosa gani la
jinai linalomzuia asipewe dhamana au ni pesa yenu ndio inaongea? Sasa ndio
utajua kuwa hii nchi siku hizi inaendeshwa kwa sheria wala sio pesa. Mwambie
mama Cote, jioni ya leo, Tunda analala nyumbani kwake. Akinisamehe, nampeleka
kanisani, namuoa kihalali. Upende usipende Bethy. Na mimi nataka kupumzika.”
“Mwanamke
maneno mpaka nje ya nyumba! Ugomvi hauishi kila siku unabadilisha visa tu!” “Huwezi
kwenda kumtoa Tunda.” Bethy akamzuia kwa hasira kali.“Watch and see!” Gabriel
akajibu kwa jeuri, akageuka na kuondoka. Wakati anaondoka mkewe akamvuta kwa
nguvu huku akimtukana. Akamchania shati.
Alipoona Gabriel hajibu kitu anaondoka,
akamvuta kwa nguvu zake zote. Gabriel akajigonga kwenye nguzo, wakati anataka
kutua sakafuni, kisogo kikajipigiza
kwenye ncha ya urembo uliokuwa umejengewa kuzunguka ile nguzo. Gabriel
alitua chini sakafuni akiwa amelala chali. Kimya. Walichoona ni damu
zikichuruzika chini ya kichwa cha Gabriel. Zilianza kusambaa na kutengeneza
dimbwi la damu chini ya kichwa chake huku amefunga macho. Bethy alishtuka sana.
Msiba mzito, Bethy amuua
mumewe.
Kilikuwa kitendo cha
muda mfupi sana, alichokifanya Bethy kwa hasira bila kufikiria. Kutoka
alipomvuta, kujigonga kichwa kwenye nguzo, mpaka kujipigiza kisogo kwenye ncha
ya kona ya urembo wa hiyo nguzo na kuwa pale sakafuni kimya amefunga macho!
Kilikuwa kitendo cha muda mfupi sana.
“Jamani
kaua!” “HaaH Kaua!” “Kaua!” “Kaua!” “Heee kaua!” Watu
wakaanza kupiga kelele na kuzidi kujaza watu pale. Hapo ndipo kila mtu akageuka
mtangazaji wa habari. Badala tu ya kuchukua video wakaanza kujichukua na wao,
wakieleza tukio zima kila mmoja kwa jinsi yake wakiripoti live kutoka kwenye
tukio.
Maaskari waliokuwa wakilinda pale
wakakimbilia pale, wakamshika Gabriel pale sakafuni ni kweli hakuwa akihema
wala hapakuwa na mapigo ya moyo. Bethy alipoona hivyo, akataka kukimbia. Watu
wakamkamata wakaanza kumpiga Bethy kama mwizi huku wakimtukana.
Ikabidi tena wale askari walinzi wa
lile jengo ambapo pembeni kulikuwa na benki waingilie kumuokoa Bethy aliyekuwa
anagaragazwa sakafuni kwa kipigo kikali. Alishachaniwa nguo zake zote, zikawa
zikining’inia mwilini mwake. Hakuwa na tofauti na kuwa uchi kwani wengine
walifanya juhudi za makusudi kumtoa hizo nguo kama kumdhalilisha.
Walimchukua Gabriel kwenye gari
akakimbizwa hospitalini, mkewe kituo cha polisi Osterbay. Kufikishwa Gabriel
mapokezi, wauguzi wakamwangalia, wakawaambia wale waliomleta na askari mmoja
wao kuwa alishafariki. Kila mtu akabaki na mshangao.
Alikuwa ni Gabriel! Kijana aliyekuwa
amefanikiwa hapo nchini. Akisaidia wenye shida mbali mbali. Sifa kubwa zaidi,
alijulikana ni mcha Mungu. Hakuwahi kuwa na kashfa, ndio kwa mara ya kwanza
siku ya kifo chake mkewe alitangaza hadharani mahusiano aliyokuwa nayo na
Changudoa, na anataka kumuacha yeye na watoto ili awe na huyo malaya, Tunda.
Kila mtu pale mapokezi akataka kujua
kilichomsibu kijana huyo. Wakaanza kusimuliana. Mwenye kuongeza lake akaongeza,
ukawa mjadala mkubwa sana pale mapokezi. Mmoja wa wauguzi akaona video ya tukio
la Gab na mkewe imesharushwa kwenye group lao la whatsapp. Akawaonyesha kuanzia
mwanzo akionekana Bethy akimtukana mumewe wakati Gabriel yupo kimya. Akaonekana
Gabriel anataka kuondoka, mkewe akamvuta kwa hasira na kumsababishia kifo.
Maneno yakaendelea pale na mwili wa
Gabriel mwenyewe ukiwa bado hapo hapo mapokezi. Kila mtu alisema lake kutokana
na ile video. Baada ya muda mfupi sana kile kisa kikasambaa kila mahali. Kila
mtandao ukaonyesha ile video. Ndipo sasa ikaanza kusambazwa ya kisa chote
kuanzia Gabriel anatoka ofisini kwa mkewe mpaka mkewe kumkimbilia nje.
Wanandoa hao wacha Mungu, walioamka
asubuhi hiyo kwenye jumba la kifahari, nakutoka hapo nyumbani na magari ya
kifahari, siku hiyo iliisha tofauti. Gabriel alipelekwa chumba cha maiti
wanakowekwa maiti zote. Waliokufa fukara na yeye tajiri akawekwa nao hapo hapo.
Walio kufa kwa kuugua kwa muda mrefu, na yeye aliyekufa bila kutajaria, akiwa
na mipango mingi hata ya siku hiyo, wote waliwekwa humo ndani wakisubiri safari
yao ya mwisho hapa duniani.
Bethy naye alifikishwa kituo cha polisi
akiwa anavuja damu, na maumivu makali mwili mzima kwa kipigo alichokipata
kutoka kwa wananchi wenye hasira kali. “Amemuua mumewe kikatili sana!” Mmoja wa
maaskari aliyekuwa anamvuta Bethy aliongea huku akimsogeza mapokezi. Wote walio
wakuta pale mapokezi wakawageukia wao. “Wapi?” “Karibu na mitaa ya Posta ya
zamani. Ni mke wa Gabriel.” “Haiwezekani!” “Amemuua Gabriel!!?” Askari mwingine
akauliza kwa mshangao mkubwa sana.
“Amemuua bwana! Ameyatoa maisha ya yule
kijana hivi hivi, mbele za watu!” Bethy alizidi kulia asijue kama ni hofu, au
maumivu. Alikuwa akitetemeka kama amepigwa na baridi. Na yeye alisukumwa
kikatili sana mpaka selo walipokuta watuhumiwa wengine.
Kwa Mchungaji!
Wakati mama Penny yupo sebuleni na
mumewe, wote wametoka kwenye shuguli zao, msichana wa kazi akawafuata akiwa
amestuka sana. “Mama Penny! Mama Penny! Nimesikia jina la anti Tunda kwenye hii
video ya huyu dada aliyemuua mumewe.” “Nani kamuua nani na wewe!? Acha kunitia
pressure bwana!” “Ona mwenyewe.” Akamkabidhi simu mama Penny. Baba Penny
akahamia pale alipokuwa amekaa mkewe.
Alianza kuonyeshwa Bethy akimtukana
mumewe. Alimtukana kwa kutaka kumuacha yeye ili amuoe Tunda. Likasikika jina la
mama Cote, kumsaidia Bethy kufanya mpango wakumfunga Tunda kwa shutuma
zinazomkabili akiwa amefanikiwa kukusanya ushahidi wote, ili yeye Gabriel
atulie na familia.
Bethy alionekana kuendelea kutupa
shutuma kwa marehemu mumewe, huku akiropoka mfululizo. Mara amtetee Tunda,
amshutumu Gabriel. Mara ajitetee yeye, amshutumu mama Cote. Akaonekana na
Gabriel na yeye akimtetea Tunda kwa mkewe na kumwambia yeye mwenyewe ndiye
aliyevunja ndoa yao asimsingizie Tunda.
Mwishowe alionekana Gabriel akitaka
kuondoka baada ya mkewe kumtukana zaidi na kumuonya asiende kumtoa Tunda rumande,
Gabriel hakuonekana kujibu tena ila kuondoka ili kuepusha shari zaidi, Bethy
akaonekana kuanza kumvuta nguo. Alifanya hivyo kama mara tatu nakufanikiwa
kumuangusha. Akaonekana Gabriel akijigonga kwenye nguzo, kona ya urembo mpaka
sakafuni akivuja damu nakupoteza maisha. Mwili wa Gabriel ulionekana umelala
pale sakafuni, damu zilionekana kutapakaa chini ya kichwa chake.
Mama Penny akarusha ile simu. “Mungu wangu,
Tunda!” Alisikika mama Penny akipiga yowe. Mikono kichwani. Ghafla
akaanza kulia kama aliyefiwa. “Naomba utulie mama Penny. Hizi habari tumepata
nusu, halafu hatujui kama ni Tunda tunayemfahamu.”
“Ni Tunda wetu, baba
Penny. Umesahau habari za Gabriel? Alinisimulia Tunda kuwa amemgeuka Net kuwa
amemchukulia mwanamke wake ambaye ni yeye. Na Gabriel alikuwa tayari kumuacha
mkewe sababu ya Tunda. Nilikwambia hiyo habari niliyokuwa nimeambiwa na Tunda. Tena
alikuja hapa amepooza sana. Ukawa unamtania lakini amenyamaza. Nilipomsindikiza
kwenye gari yake ndipo akaniambi kuwa wamemgeuka Net. nakunisimulia kila kitu.
Umesahau?” “Sasa hivi ndio nakumbuka. Mungu amsaidie yule mtoto. Sijui
atakuwa amefungwa wapi!?” Tayari hali ya pale ikageuka majonzi.
“Kweli yule mama
ameshindwa kabisa kumsamehe Tunda, mpaka amemfungulia mashitaka jamani!”
“Tena akiwa amekwenda kutubu kanisani! Hakika Mungu hatamuacha.” Mchungaji
akaongeza akionekana kuumia zaidi. Wasijue mkasa mzima uliompata Net ambaye yu
taabani huko nchini kwao, na Tunda huko gerezani. “Sasa
na Net yuko wapi?” “Inamaana wamemkamata leo huyo Tunda?” Yakawa maswali
juu ya maswali yasiyo na majibu. Wakaanza kupiga simu ya Tunda na Net bila
mafanikio.
Mama Penny na mumewe waanza
kumsaka Tunda.
Kesho yake asubuhi kitu cha kwanza
wakaenda kituo cha polisi cha pale pale Tabata kuulizia kama Tunda anaweza kuwa
wapi. Wakawaambia polisi mara ya mwisho Tunda na mumewe walikuwa kwenye
fungate. Wakaeleza kwa kifupi kuwa wao ni wachungaji na Tunda ni mshirika wao.
Habari zile za mauaji yaliyotokea siku iliyopita walisikia Tunda kutajwa kuwa
amefungwa.
“Lakini kwa jinsi ilivyo sasa, kwa kosa
lolote wanaweza wakamnyima dhamana, kwa ajili ya usalama wake binafsi. Maana
yeye anaonekana ni kama chanzo cha ugomvi.” “Ni wivu tu wa maswala ya mapenzi.
Tunda hakuwa na mahusiano na Gabriel.” Wakajaribu kueleza bila kutoa mambo ya
Tunda ya zamani.
Mchungaji alijieleza kiungwana sana
mpaka wakamuelewa. Mmoja wa wale askari akawasaidia kupiga simu kwa rafiki
yake, baada ya muda akapewa jibu kuwa Tunda atakuwa yupo gereza la Keko.
Mchungaji na mkewe wakashukuru na kutoka pale kuelekea gereza la Keko.
Gerezani Keko.
Walifika pale, wakaandikisha majina.
Wakakuta watu wengine wakizungumza na mahabusu wengine. Na wao wakakaa. Baada
ya muda Tunda akatolewa. Alipowaona tu, akaanza kulia. Tunda alilia zaidi ya
nusu saa. Alilia. Akalia bila kunyamaza. “Ni nini kilitokea Tunda?” Mchungaji
akauliza, lakini Tunda alishindwa kujibu.
“Net yuko wapi?” Akaendelea kuuliza
lakini Tunda alikuwa akilia na mkewe naye analia. “Mama Penny naomba nyamaza
bwana ili tuweze kuzungumza na Tunda!” Wote wawili waliendelea kulia.
Baada ya muda, wakashangaa Tunda
ananyanyuka na kurudi ndani bila kuongea chochote ila kulia tu. Alikuwa akilia
kwa kwikwi huku amejifunika uso. Wakabaki pale mama Penny akilia na mumewe ametulia
hajui chakusema tena. Walikaa pale wakisubiria labda Tunda angerudi, lakini
hakurudi mpaka muda ulipoisha na kutakiwa waondoke. Mchungaji akamnyanyua
mkewe, wakaondoka.
Mama yake Gabriel Naye.
Siku hiyo kabla yakuisha tena, kukazuka
habari yakuhuzunisha zaidi. Mama yake Gabriel afariki kwa mshtuko. Habari
zilieleza kuwa baada ya mama huyo kupata habari kuwa mtoto wake amekufa, hapohapo
alianguka na kupoteza fahamu kwa mshtuko.
Alikimbizwa hospitalini. Juhudi za
kuokoa maisha yake hazikufanikiwa. Yule mama hakuzinduka mpaka saa kumi
alfajiri siku inayofuata, mashine zilipoonyesha amefariki. Familia hiyo ilikuwa
na msiba mzito ulioinua simanzi kwa wengi. Mama na mtoto wake! Tena ni Gabriel
kipenzi cha wengi!
Gerezani.
Tunda aeleza Yote na kuweka kikomo.
Kesho yake wakarudi tena mahabusu
kumuona Tunda. Lakini safari hii walifika na mama yake Tunda. Wakajiandikisha
kama jana yake, wakakaa wakisubiri Tunda aitwe, wakijua labda siku ile atakuwa
ametulia. Lakini alirudi yuleyule askari aliyekwenda kumwita na barua mkononi.
‘Mama Penny na mchungaji,
nawashukuru sana kuwa na mimi kwa miaka yote hiyo. Mlinipa familia ambayo
sikuwahi kuwa nayo. Nakushukuru mama Penny, kufanyika dada ambaye sikuwahi kuwa
naye wala kudhani nastahili kuwa na dada wa aina yako. Lakini nawaomba kwa sasa
msinifuate tena hapa. Msije hapa. Haya ni mapito yangu binafsi, ambayo siwezi
kuruhusu na nyinyi kuingia doa.’
‘Sasa hivi ninasakwa na watu
wengi ili tu kumfahamu Tunda waliyemsikia kwenye ugomvi wa marehemu Gabriel na
mkewe. Sitaki nyinyi niliowakuta na sifa nzuri, tena mnamajukumu ya roho nyingi
za watu wanao wahitaji, kupotea au kuangamia na mimi mtu mmoja tu! Hapana.
Tafadhali naomba msifike tena hapa, ila mniombee tu.’
Tunda akaendelea kuandika.
‘Siku ile baada ya kuagana pale
kwenye harusi yangu na Net, tulikwenda Resort, kama alivyowaambia Net. Siku ya
jumapili asubuhi, tuligongewa na askari polisi, walituamuru tutoke pale twende
kituo cha polisi. Tulipokuwa tukipakizwa kwenye gari la hao polisi, nje ya ile
resort, alikuja mama Cote. Alitusomea mashitaka yetu. Naomba niwaeleze makosa
ya kwangu tu. Na ninafanya hivi kwenu kwa ule umbali mliofika na mimi kwenye
maisha yangu.’ Mchungaji aliendelea kusoma kwa sauti ya kusikika kwa wao
watatu tu.
‘Nimeshitakiwa kwa makosa
matatu. La kwanza ni kumuoa Net. Mama Cote amenishitaki akidai ni moja ya njia
ninazotumia kumrubuni Net ili kumvuta upande wangu, kwa sababu ambazo
alizitaja. Ameita au amenishitaki kwa kosa la kuendeleza biashara ya ngono. Kwa
bahati mbaya sana, yule mwanasheria tuliyemuamini kutukamilishia makaratasi
yetu, ili kukamilisha taratibu zote kabla ya ndoa, aidha kwa kutokujua au kwa
makusudi, hakukamilisha taratibu kama ilivyotakiwa.’
‘Kwa kifupi, mama Cote
alituambia ndoa yetu haitambuliki kisheria hapa nchini, kwa hiyo nayo ni ushahidi
kuwa mimi nimetengeneza uongo, ili kuolewa na Net, ambaye siye raia wa nchini
Tanzania. Anao ushahidi mwingi tu, na kwa kuwa anaonekana ameweza kumfikia yule
mwanasheria tuliyemlipa atusaidie maswala yote ya ndoa, amesema huyo
mwanasheria atatoa ushahidi, utakaonishitaki mimi kuwa ni kama nilikiuka sheria
ya ndoa za kimataifa, nakudanganya ili kuweza kuolewa na Net, kujirahisishia
njia yakutumia au kumiliki mali ya kampuni yake. Kwa vipi au ni ushahidi gani
watatoa siku hiyo ya mahakamani, sielewi. Ila wanaonekana wamejipanga vizuri.’
Mchungaji akaendelea kusoma.
“Kosa la pili ambalo ni kweli
nililifanya kwa hiari yangu nikitaka kumsaidia Net, ni juu ya ile nyumba yake
ambayo ilikuwa kwa jina la kampuni ya yule mama. Nakumbuka mama Penny na
mchungaji mlituonya sana, lakini Net alituambia ni jasho lake asingependa lipotee.
Mimi nikakubali kununua kwa pesa ambazo alinipa Net mwenyewe.’
‘Mama Cote anadai ile nyumba ni yake. Hata hati ya
nyumba ambayo Net alikuwa tayari ameshajaza fomu huko wizara za aridhi,
kubadilisha jina iwe kwa jina langu, ilikuwa kwa jina la kampuni ya yule mama.
Na mbaya zaidi anao ushahidi wa makaratasi yote ambayo Net alijaza habari zangu
zote akiwa ananiuliza maswali huku anajaza hizo karatasi za kununua nyumba, na
kubadili hati ya nyumba. Na mwishoni mimi niliweka saini kote. Net kama mfanyakazi
tu wa ile kampuni, kisheria haruhusiwi kuniuzia mali ya kampuni bila idhini ya
mmiliki wa kampuni ambaye ni mama Cote.’
‘Sasa mama Cote amenishitaki kwa
kosa la kutumia rushwa ya ngono, kumrubuni mfanyakazi wake wakigeni, asiyejua
sheria za aridhi hapa nchini. Si mume tena, kwakuwa ameshatusainisha talaka,
hiyo nayo ni habari ingine. Anataka kuhakikisha hiyo ndoa haitambuliki wala
haina ushahidi popote kule, hataki ijulikane hata kama ilisha wahi kutokea.
Ametupokonya kila kitu mpaka pete za ndoa.’
‘Turudi kwenye kosa la nyumba.
Kwa hiyo amenishitaki kwa kutoa rushwa ya ngono au kuuza ngono ili kupewa
nyumba ya kampuni yake. Ukiangalia ni atashinda tu. Maana ni wapi nyumba
inauzwa kwa milioni tatu!? Hakuna inapoonyesha kama Net ndio mmiliki. Na
kisheria, Net haruhusiwi kumiliki mali yeyote hapa nchini kwa kuwa sio mzawa.
Basi, kweli makosa ni yangu.’ “Mungu wangu huyu mama!”
Alisikika mama Penny aliyekuwa akilia.
“Sijui kwa nini hili jambo lilikuwa
likinisumbua sana! Hata baada ya Net kulazimishia siku ile, unakumbuka usiku
wake nilikuamsha na kukwambia hili jambo ni la kuombea?” “Nakumbuka baba Penny! Lakini Tunda alifanya kwa mapenzi,
kumridhisha Net.” Mama Penny akajibu akimtetea Tunda.
“Hebu tumalizeni kwanza hii barua,
ndipo tujadili.” Akamalizia mama Tom, au mama yake Tunda. Wakaamua kuendelea.
Mchungaji anasoma, mama Penny na Mama Tom wanasikiliza.
‘Kosa la tatu au la mwisho kwa
hapa, ni biashara hiyo ya ngono sasa. Mama Cote kwa kushirikiana na Bethy,
wanaonekana wamelipa mtu aliyeweza kuingia kwenye simu zangu za zamani. Ameweza
kuprinti au kutoa mawasiliano yangu yooote yazamani. Malipo niliyokuwa
nikipokea kwa kutumia mtandao na jumbe zangu zote kama ushahidi wa kunishitaki
juu ya biashara ya ngono.’ “Huyu mama amemkosea Mungu kwa hakika! Ametumia ukiri wa
madhabahuni kwa Mungu kumuangamiza Tunda! Hakika Mungu hatawaacha.”
Alisikika mama Penny.
‘Kwa kumalizia kisa kizima,
alituambia ili mambo yaishe, nilazima kusaini karatasi za talaka. Na niandike
kuwa naachana na Net, nikiwa sitaki kitu chochote kutoka kwake. Na karatasi
nyingine aliyokuwa ameonyesha kuwa ile nyumba inarudi kwake au kampuni yake
yeye mama Cote. Ilinibidi mimi kufanya kama alivyotaka. Tulikuwa kwenye hali
mbaya, sina jinsi nikasimulia mtu akaelewa. Tulitolewa kwenye usingizi.
Tukatolewa pale chumbani na pingu huku tukisindikizwa na askari wanne!’ “Mama anadhambi huyu!” Alisikika mama Penny tena huku akifuta
machozi.
‘Basi, baada yakufanya yote
aliyoyataka, tukijua tupo huru, mimi nilitolewa kwenye gari moja na polisi
nakuhamishiwa kwenye gari nyingine. Net akiwa analia sana, nilimsikia
akimuuliza mama yake, kwa nini wananichukua tena wakati nilifanya kila
alichotaka! Nilichosikia yule mama akijibu, alisema kuwa, yeye alikuwa pale kwa
ajili ya mali zake, amezipata. Maswala ya biashara haramu ya ngono, ni mimi
kupambana na sheria ya Tanzania. Hausiki tena. Basi, niliondoka pale, nakumuacha
Net na mama yake. Mimi nikapelekwa kituo cha polisi Kawe.”
‘Lakini chakushangaza, nilipofikishwa kituoni, nilisomewa mashitaka
yote kama yalivyo, halikuachwa hata moja.
1. Kumrubuni raia wa
kigeni, kwa kumuwezesha kuishi hapa Tanzania, kwa kumwingiza kwenye ndoa feki ili kujinufaisha na mali zake na
za mama yake.
2. Wizi. Hapa habari
ikabadilishwa tena. Ikaonekana niliiba hiyo hati ya nyumba kutoka kwa kijana
wake. Na kuibadili hiyo hati ya nyumba kutoka kwa kampuni ya Cote, iwe kwa jina
langu mimi. Na mwisho kabisa,
3. Biashara ya
ngono.
Kwa hiyo ndiyo hayo makosa matatu yanayonikabili kwa
sasa.’
“Kama ulivyosema mama Penny. Huyu mama
anacheza pabaya sana. Hajui vita yake haikuwa juu yake na Tunda, bali na Mungu.
Mungu atamchapa mama Cote, mpaka atajua kuwa Mungu anamuadhibu. Yeye mama
anayejua nguvu ya msamaha, kusamehewa dhambi, na kutakaswa, leo anatumia siri
za madhabahuni kumuhukumu Tunda! Hakika Mungu hatamuacha.” Alisikika mchungaji
akiongea kwa kuumia sana. “Mimi ndio sielewi kabisa. Itabidi tukitoka hapa
mkanielezee kila kitu.” Alikuwa mama Tom. Mchungaji akaendelea kusoma kwa sauti
ya juu kiasi.
‘Jamani, hayo makosa yote,
nilifanya. Iwe kwa kutokujua au kujua, niliyafanya. Wameyatengenezea mkasa
mkubwa sana, ambao waliniambia siwezi kupewa dhamana. Nimekaa hapa muda wote
huo, nikimlilia Mungu mliyeniambia amenisamehe, basi anitetee hata mbele za
watu. Nimetubu kwa machozi, nimekosa. Nimepoteza kila kitu. Nipo hapa peke
yangu, lakini najua Mungu hataniacha. Sijui kilichoendelea kwa Net na mama
yake. Ila kwa kifupi, Net si mume wangu tena. Yule mama alihakikisha nasaini
talaka, na kujitenga na mali zao na kunipokonya pete zote mpaka ya uchumba.’
“Jamani Tunda wangu!” Alisikika tena mama
Penny.
‘Najua mngetamani kunisaidia.
Lakini sidhani kama mtaweza. Naomba msaada wa maombi tu. Ili hiyo siku
nitakapoitwa mahakamani, basi, yeye mwenyewe Mungu, akajidhihirishe huko. Mimi
sijui hata pakuanzia kujitetea, kwa kuwa nilikosa. Kuna ushauri walinipa hawa
askari wa hapa, kwa sasa nitulie tu hapa ndani. Kifo cha Gabriel kimeshtua watu
wengi sana. Mimi wamenionyesha wao wenyewe, wakanishauri vizuri tu. Kuwa kwa
sasa, hapa nilipo nisehemu sahihi hata kwa usalama wangu.’
‘Japo ni kama wananipa moyo
kuwa, Gabriel alifanyika mtetezi wangu. Kabla ya kifo chake, kwenye ile video,
anaonekana alikufa akinitetea. Lakini, wameniambia, Bethy anao ndugu na wazazi.
Siwezi kujua wao watachukuliaje hilo. Bethy anaonekana amesababisha kifo cha
mumewe, akiwa anamzuia asinitoe mimi huku jela. Haya, na hiki kifo cha mama
yake Gabriel naye! Imekua balaa juu ya balaa na ilionekana sababu au chanzo ni
mimi. Bethy akipigania ndoa yake. Wapo ambao watakuwa na hasira na mimi tu. Ni
heri nitulie hapa kwanza. Sina jinsi ila kutulia. Maana hilo nalo limekuwa
tatizo la nne. Ni kama nimesabisha kifo cha Gabriel ambacho kimepelekea kifo
cha mama yake pia.’ Kilisikika kilio cha mama Penny.
Baba Penny akaendelea. ‘Tafadhali nawasihi sana, najua mnao na watawajia kina Tunda wengi
sana kwenye maisha yenu, msiharibu huduma yenu kwa ajili yangu. Kama mnamwamini
Mungu, naombeni mkae mbali na hapa, mpisheni Mungu afanye kwa namna yake.
Sitaki chochote au ushiriki wenu kwangu na Net, ujulikane kwenye vyombo vya
sheria au hata mitandaoni. Ninachomshukuru Mungu, ni kama nilimsikia mama Cote
akisema aliwahi video zote na picha zote za harusi. Anavyo yeye. Kwa hiyo
naamini mtakuwa salama kwa muda, mpaka mambo yakae sawa. Na ukweli utambulike.’ “Tunda
anasahau yeye kwetu sio mshirika tu. Ni ndugu sasa.” Aliongeza baba Penny akiwa
na majonzi.
“Hata hivyo, ni mchungaji gani
anayechunga kondoo asichafuke? Sisi tunachunga wenye dhambi. Ndio wito
aliotuitia Mungu. Kuwasogeza wenye dhambi karibu na Mungu. Hatuna chakujificha
kwa yeyote.” Aliongeza mchungaji. Mama Tom akabaki akiwashangaa wanavyotaka
kujiingiza kwenye lawama!
‘Mama Penny, najua nimeacha gari
yangu kwako na vitu vyangu vyote nyumbani kwenu. Nakusihi sana, uendelee kufuatilia
kesi ya baba yangu. Lipo tumaini la kutoka kwake jela. Nilibakisha malipo
kidogo kwa yule wakili wake. Naomba uwasiliane na huyo wakili, tumia pesa yangu
umlipe hicho kiasi atakachokwambia. Mwambie kisibadilike kitu. Hakikisha baba
anatoka jela. Tafadhali dada yangu. Sitaki baba yangu aje afie jela.’
‘Siku ya kumtizama, naomba
ukamwangalie ujue anaendeleaje. Walimtoa hospitalini, sijui atakuwa amepona au
bado, nilimuacha bado mwili hauna nguvu. Naomba umfuatilie mpaka atoke.
Akitoka, naomba umtunze kidogo mpaka apate nguvu. Najua nakupa mzigo mzito,
lakini nakusihi dada yangu, nisaidie. Hana pakwenda. Nilipanga akitoka,
apumzike kidogo, arudishe nguvu na mawazo, ndipo umpe mtaji. Zungumza naye ili
kujua nini anataka kufanya. Mtolee pesa kwenye akaunti yangu ya akiba, mpe,
mtafutie chumba, mlipie kodi hata ya miezi sita tu, aanze maisha. Naamini hata
mwezi ujao, atatoka jela kama si mapema na hapo.’ Mama
Tom akawa amechanganyikiwa zaidi.
“Kwani Yohana alifungwa na yeye!?”
Akauliza mama Tom, wote wakamgeukia. “Mimi sikuwa nawasiliana naye kabisa. Hata
habari zake sikuwa nazo tena. Alishanikera yeye na yule mkewe mwenye roho kama
ya shetani! Mkewe alimpiga Tunda karibu ya kumuua, na yeye Yohana alikuwa
akiishi humo humo ndani! Nikamuona ni mpuuzi anayetawaliwa na mkewe, sikutaka
hata kumsikia tena.” Akajitete mama Tom, nakumuudhi zaidi mama Penny.
“Sasa anatofauti gani na wewe
uliyemuacha Tunda akibakwa kila siku na mumeo, na wewe ulikuwa ukiishi humohumo
ndani? Huogopi kusema! Kwanza wewe ndiye uliyemsababishia Tunda matatizo yote
haya. Mama gani unashindwa kujua kama mtoto wako wa kike anabakwa! Upuuzi gani
huo!?” “Majukumu mama Penny.” Akajaribu kujitetea nakuharibu zaidi.
“Acha kujitetea ujinga! Umenunua
ulimwengu sasa hivi? Mbona wenzako tunafanya kazi na tunalea? Watoto wako
wakike wote wawili walikuwa wanabakwa na mumeo humohumo ndani halafu unajitetea
ujinga! Msichana wako wa kazi karibia auwawe kwa kubakwa na mwanaume huyohuyo
na wewe upo nyumba hiyo hiyo halafu sasa hivi unaongea nini? Nitakupiga mimi sasa
hivi hapa.” Mama Penny alikuwa amekasirika anatetemeka karibu amrukie.
“Mama Penny naomba utulie.” Mumewe
akamtuliza. “Huyu ndio chanzo cha yote haya! Amemsababishia Tunda matatizo
ambayo hawezi kumsaidia. Wewe mtoto wa kwanza umejua alikuwa akibakwa.
Halafu..” “Sikuwa najua mama Penny. Naomba usinilaumu. Mimi nilichojua ni kuwa
Tunda alianzisha mahusiano na...” “Nitakupiga mama Tom acha kujitetea ujinga
wewe!”
“Wewe mtoto wako wa kike unaishi naye
humo humo ndani, hujui chochote kwenye maisha yake, mpaka unakuja kumgundua
mjamzito! Kana kwamba haitoshi, umempeleka hospitalini kwa nguvu, wewe na
manesi wenzako sijui daktari mkamchoma sindano. Unapata habari kutoka kwake
akiwa na madawa ya usingizi! Ulivyo mshezi wewe, ukamtoa mimba mtoto wako
wakumzaa wewe mwenyewe kwenye starehe zako. Ukamtelekeza hospitalini anavuja
damu, halafu wewe ukaanza kupita kwenye majumba ya watu unamuharibia mwanao
sifa!” Kimya.
“Ulifikiria au ulitegemea aende wapi
kama sio kufanya biashara ya elimu ya ngono aliyomfundisha mumeo tangia yupo
mtoto mdogo? Ameanza kumbaka Tunda tokea hajavunja ungo mpaka amevunja ungo,
anamlala binti yako na wewe upo palepale, mshenzi wewe. Halafu bila huruma
ukamtupa!”
“Usimfukuze mumeo, ukamfukuza mtoto
mdogo! Kana kwamba haitoshi, mwanaume huyohuyo ukamuachia mtoto wa watu
uliyemtoa kijiji. Kambaka mpaka kutaka kumuua. Mpumbavu wewe, mshenzi usie na
akili, unamrudisha yule mtoto kijijini kwao kashageuzwa tahira na mumeo, ukaona
mkabidhi mumeo mtoto mwingine wa kike awe anamchezea wakati wewe unazungusha
kiuno kutafuta pesa.”
“Kamchezea mtoto mpaka kampa gonorea,
mtoto ananuka ndio mama unashtuka, mshenzi wewe. Huna aibu umekuja hapa
kumsanifu Tunda! Na unaonekana kama sio kufukuzwa na ndugu za mume, usinge..”
“Mama Penny! Mama Penny! Naomba tulia kidogo. Tulia mama. Huko unakokwenda
utashindwa kurudi. Tafadhali tulia.” Mumewe akamsihi.
“Nimemuomba Tunda msamaha. Na
ameniambia amenisamehe.” “Basi msubiri huyohuyo Tunda atoke jela ili akusaidie.
Nisiione sura yako nyumbani kwangu. Nishakuelekeza kupamba, Tunda
ameshakutafutia chumba. Amekupa vitu vyake vyote vya ndani na pesa ya mtaji,
nenda kaanze maisha. Na usipobadilika na yule mwanao wa kiume watamlawiti
wakati unahangaika kutafuta pesa.” Mama Penny akaendelea.
“Na kama ulivyosikia, Tunda yupo
Tanzania. Haondoki tena, ipo siku atatoka tu jela. Nakuja kuchukua vitu vyake
vyote vyabiashara, namtunzia. Akitoka, anaendelea na biashara yake. Ushamuharibia
maisha yake, sitaki aje atoke jela aanze maisha upya. Na ile ofisi pia sio
yako. Kwa kuwa amelipia kodi ya mwaka, naenda kumtafuta mteja mwingine,
napakodisha, pesa namuwekea benki. Yaani unapotoka hapa, ujue upo kivyako.
Nisiione sura yako tena. Haya kwenda.” Mama Penny alijisahau yupo gerezani.
Watu wote wanawasikiliza.
“Unajidai ulimuomba Tunda msamaha baada
ya Tunda kufanikiwa na kuwafuata yeye mwenyewe! Mbona wakati anashida
hukumtafuta umuombe msamaha? Alihangaika kufanya kazi usiku kucha na mchana,
akitafuta pesa kukutunza wewe uliyeharibu maisha yake! Baba ambaye hata hakuwa
akimfahamu ndiye aliyemsaidia, tena wewe ukiwa unamkataza baba yake na wanao
mzunguka wasimsaidie Tunda, leo unamtukana baba yake! Mjinga kabisa. Sasa
nikuone karibu na vitu vya Tunda. Na mimi nitakufungulia mashitaka wewe kwa
kumtoa mimba Tunda. Uliua kiumbe cha Mungu. Toka kabla sijaanzisha kesi
nyingine mimi.” Askari magereza akawasogelea. Walianza taratibu, lakini baadaye
mama Penny akashindwa kujizuia. Wakatolewa wote nje.
Mambo yanazidi kuwa mambo. Jambo juu ya jambo.
Njama zakumuangamiza Tunda zimeishia tofauti. Lengo ilikuwa awapishe
mtaani. Lakini imeisha tofauti. Kaburi walilomchimbia Tunda nani analia sasa
hivi?
⮚
Msiba mzito kwa kina Gabriel.
⮚
Bethy ameishia mikononi mwa polisi kwa kosa la kumuua mumewe
kikatili.
⮚
Kifo cha Gabriel kimesababisha kifo cha mama yake.
⮚
Mama Cote amekimbia. Hapatikaniki.
⮚
Tunda yupo jela kwa makosa matatu yenye ushahidi.
⮚
Hakuna anayejua kama Net yupo mahututi hospitalini. Na hata wauguzi
wameshindwa kumtambua.
⮚
Ndoa iliyofungwa kama kwa siri hivi na mchungaji akiwa msitari wa
mbele pamoja na familia yake, haitambuliki kisheria. Mama Cote anao ushahidi
akitaka kufuta kabisa hiyo ndoa isijulikane wala kutambulika kisheria. Itakuaje
kwa watu wakijua ushiriki wa mchungaji kwenye aina hiyo ya ndoa yenye tuhuma
nzito?
⮚
Safari hii Tunda anatoka vipi? Net? Mama Cote je? Kanisa
wanalochunga baba Penny na mkewe! Bibi Cote naye? Endelea kusoma...
0 comments: